Thursday 30 March 2017

UZINDUZI WA MAFUNZO YA UTENGENEZAJI WA TOVUTI ZA SERIKALI KWA MIKOA YA MTWARA, LINDI NA RUVUMA







Katibu tawala wa mkoa wa mtwara ndugu Alfred Luanda akifungua  mafunzo ya utengenezaji wa tovuti za serikali kwa Mikoa  ya Lindi, Mtwara na Ruvuma yaliyofanyika mtwara kuanzia tarehe 20 hadi 27 machi, 2017



 
Uimarishaji wa mifumo ya sekta za umma kupitia  mradi wa PS3 ikiwemo uanzishwaji na uhuishwaji wa Tovuti katika taasisi za umma utasaidia  serikali kuimarisha utoaji wa taarifa kwa umma kwa haraka na kwa wakati hali itakayo boresha utawala bora katika kuwahudumia wananchi kwa uwazi.

Hayo yamesemwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara ndugu Alfred Luanda wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya utengenezaji wa tovuti za serikali kwa mikoa  ya Lindi, Mtwara na Ruvuma yaliyofanyika kwa muda wa siku nane kuanzia tarehe 20 hadi 27, Machi, 2017 na kueleza kuwa mafunzo hayo yatawajengea uwezo Maafisa Habari na TEHAMA kuweza kuendesha tovuti za serikali vizuri katika kuwahabarisha wananchi. 

Luanda amewaeleza washiriki kuwa uboreshaji wa tovuti za serikali utawezesha wananchi kupata fursa na haki ya kupata habari na taarifa kwa njia ya mtandao  ambayo ndio njia ya haraka zaidi.

“Mnapaswa kufahamu kuwa upatikanaji wa taarifa kwa umma ni suala la kisheria, hivyo baada ya mafunzo haya mtakuwa mmepata uwezo zaidi wa kuandaa na kutangaza taarifa na fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo kwenye taasisi zenu”  alifafanua Luanda 

Uimarishaji wa mifumo ya sekta za umma unaofadhiliwa na shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) ulianza mwaka 2016 na utadumu kwa miaka mitano (5) ambapo jumla ya Halmashauri 93 katika mikoa 13 ya Tanzania bara pamoja na serikali kuu zitanufaika.

No comments:

Post a Comment